Search for a command to run...
Implikecha ni suala ambalo hujitokeza katika mazungumzo miongoni mwa washiriki katika mchakato wa mawasiliano. Kulingana na Grice (1975) ni kwamba implikecha ni kile kinachomaanishwa na msemaji wa kauli fulani japo hakijitokezi waziwazi kwa mujibu wa maneno yaliyotumiwa. Makala hii inadhamiria kubainisha mchango wa implikecha katika kukuza maudhui na hivyo kufanikisha msuko wa drama. Utafiti huu utaongozwa na nadharia ya umaanisho ya Grice (1975). Utafiti huu ulihusisha sampuli lengwa ambayo ni tamthilia ya Kifo Kisimani. Tamthilia iliteuliwa kutumika katika utafiti huu kwa kuwa tamthilia husukumwa mbele na dayolojia ya wahusika na hivyo huakisi matumizi halisi ya lugha katika mitagusano ya kila siku ya wanajamii. Data iliyotumiwa katika utafiti huu ilipatikana kwa kusoma kwa makini tamthilia nzima ya Kifo Kisimani na kunakili kauli zote zilizoonyesha ukiukaji wa kanuni za ushirikiano za Grice (1975). Kila mara kanuni za Grice zinapokiukikwa hujitokeza maana ya msemaji ambayo Grice huita umaanisho au implikecha. Data ya utafiti huu ilichanganuliwa kwa njia ya maelezo kwa kuongozwa na kanuni za ushirikiano ambazo ni pamoja na: kanuni ya namna, kanuni ya ukweli, kanuni ya idadi na hatimaye kanuni ya uhusiano. Utafiti huu utasaidia katika kuelewa suala la umaanisho kama mkakati wa kuendeleza drama. Hili ni muhimu kwa kuwa tamthilia zinapoandikwa hukusudiwa kuigizwa jukwaani na hivyo huakisi matumizi halisi ya lugha miongoni mwa wanajamii. Hivyo migogoro ya wahusika husaidia kusukuma msuko wa drama mbele kwa kuwa huwa kama jira ya matendo yao na mitagusano yao mbalimbali. Utafiti huu utaichangizia nadharia ya ushikiriano kimaarifa na hivyo kuipanua zaidi kimawanda kwa kuitumikiza.
Published in: East African Journal of Swahili Studies
Volume 9, Issue 1, pp. 132-140