Search for a command to run...
Lengo la utafiti huu lilikuwa kuchunguza jinsi nyimbo pendwa za mwanamuziki Ken wa Maria zinavyoendeleza utaifa wa jamii ya Akamba. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kupambanua changamoto zinazokumba utaifa wa jamii ya Akamba kwa mujibu wa nyimbo pendwa teule za Ken wa Maria. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya utaifa iliyoasisiwa na David Smith. Nadharia ya utaifa hueleza kwamba ili utaifa wa jamii uwepo lazima jamii hiyo iweze kumiliki utamaduni mmoja, lugha, imani ya dini na historia. Mihimili ya nadharia hii ndiyo iliyoelekeza utafiti huu wakati wa kukusanya, kuchanganua na kuwasilisha data kwa kuzingatia madhumuni ya utafiti. Muundo wa utafiti huu ni muundo elezi. Utafiti huu ulifanyiwa katika maktaba ili kupata data. Utafiti huu ulitumia data za sekondari kutoka majukwaa ya kidijitali. Sampuli ya kimakusudi ilitumika ili kupata nyimbo 24 ambazo zilipakuliwa kutoka mtandao wa YouTube na Mdundo.com. Nyimbo hizi zilitafsiriwa katika lugha ya Kiswahili kisha kuchanganuliwa ili kubainisha changamoto zinazokumba utaifa wa jamii ya Akamba kwa mujibu wa nyimbo pendwa za Ken wa Maria. Data ilichanganuliwa na matokeo yake kufafanuliwa kwa kutumia mbinu ya kimaelezo. Uwasilishaji wa data ya utafiti ulifanywa kwa njia ya kimaelezo. Utafiti huu ulibaini kwamba utaifa wa jamii ya Akamba unakumbwa na changamoto kama vile kuzuka kwa utambulisho mpya, utandawazi, uhamiaji, siasa za utengano pamoja na usaliti wa kisiasa. Utafiti zaidi unaweza kufanywa kuhusiana na mada hii hasa jinsi wasanii wengine kutoka jamii ya Akamba wanavyotalii suala la ujenzi wa utaifa wa jamii pamoja na changamoto zake
Published in: East African Journal of Swahili Studies
Volume 9, Issue 1, pp. 236-251